KUNDO AKAGUA MRADI W...
KUNDO AKAGUA MRADI WA MAJI URAMBO, TABORA ATANGAZA NEEMA YA MAJI KWA WANANCHI WA MAENEO HAYO.
03 Mar, 2025
KUNDO AKAGUA MRADI WA MAJI URAMBO, TABORA ATANGAZA NEEMA YA MAJI KWA WANANCHI WA MAENEO HAYO.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amefanya ziara katika Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, ambapo amekagua utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28, ambao unatarajiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Urambo, Kaliua, na Sikonge.

Katika ziara yake, Mhandisi Kundo amekutana na Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamis A. Mkanachi, ambaye alieleza kuwa Mkoa wa Tabora, hususan Urambo, unakabiliwa na changamoto kubwa ya maji.

Hata hivyo, amefafanua kuwa tatizo hilo litatatuliwa kupitia mradi wa miji 28, ambao utahusisha usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi kwenye miji hiyo.

Mhandisi Kundo amekagua ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni 2,000,000 lilipo katika mji wa Urambo, pamoja na tenki jingine lenye ujazo sawa lilipo katika mji wa Kaliua.

Aidha, amefahamishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (TUWASA), Eng. Mayunga Kashilimu, kwamba utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 60 kwa tenki la Urambo, na asilimia 35 kwa tenki la Kaliua.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Kundo, amemtaka mkandarasi wa mradi, kampuni ya Megha Engineering and Infrastructure Ltd, kuhakikisha kuwa anatekeleza mpango wa dharura kwa kuunganisha mtandao wa maji kutoka kwenye tenki za Urambo na Kaliua, ili wananchi waanze kupata maji kabla ya kumalizika kwa ujenzi wa matenki.

Amesisitiza kuwa kazi hiyo ifanyike kwa haraka na kuongeza nguvu kazi ili kutimiza matarajio ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Mhandisi Kundo ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo mkoani Tabora, zikiwemo bilioni 143.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa miji 28.

Amesema kuwa fedha hizo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama.

Mhandisi Kundo ametoa pongezi kwa watumishi wa sekta ya maji mkoani Tabora kwa ushirikiano wao na juhudi zao katika kutekeleza mradi huo. Aliwashauri waridhike na nafasi zao na kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kwani madaraka ni mpango wa Mungu.