HAFLA YA UTIAJI SAIN...
HAFLA YA UTIAJI SAINI MKATABA WA MRADI WA UJENZI WA MABWAWA YA KUTIBU MAJITAKA YANAYOKUSANYWA KWA NJIA YA MABOZA (SLUDGE PONDS) MANISPAA YA TABORA TAREHE 22/02/2023
22 Feb, 2023
HAFLA YA UTIAJI SAINI MKATABA WA MRADI WA UJENZI WA MABWAWA YA KUTIBU MAJITAKA YANAYOKUSANYWA KWA NJIA YA MABOZA (SLUDGE PONDS) MANISPAA YA TABORA TAREHE 22/02/2023

Leo tarehe 22.02.2023 Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora imetia saini Mkataba wa ujenzi wa Mabwawa ya kutibu Majitaka yanayokusanywa kwa njia ya Maboza katika Manispaa ya Tabora, ambapo mradi huu utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni  1.628,830,289.76 na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 kwa ukamilifu wake na unatekelezwa na Mkandarasi PERITUS EXIM PRIVATE LIMITED ya Dar- es – salaam.

Mwakilishi wa Wizara, Eng. Loishiye L. Ngotee (Aliyesimama) ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya maji ameeleza kuwa hali ya sasa ya uondoaji wa Majitaka Tanzania inafikia asilimia 16 tu ambapo Wizara imeweka mikakati ya kuhakikisha inafikia asilimia 30 ifikapo 2025 kwa kutekeleza Miradi ya ujenzi wa mabwawa ya majitaka katika miji mitano(5) ambayo ni Igunga, Njombe, Singida, Chato na Tabora. Amewataka wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza kwa wakati miradi hii.

Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Eng. Mayunga A. Kashilimu alieleza kuwa Mradi huu utasaidia wananchi wa Manispaa ya Tabora kwa kiasi kikubwa kiafya, kilimo cha umwagiliaji na kimazingira kwani mtandao wa majitaka uliopo  ni asilimia 8 pekee na mabwawa yaliyopo yamechakaa hayawezi kutibu majitaka. Asilimia 91.6 ya wananchi hutumia vyoo vya shimo ambavyo msimu wa mvua hujaa sana na kulazimika kuondoa uchafu huo kwa kutumia magari ya majitaka kutokana na kuwa asilimia 80 ya majisafi yanayotumika hubadilika na kuwa majitaka.

Aliendelea kueleza kwamba kazi zitakazofanyika eneo la Milambo Balacks ni ;-

  1. Ujenzi wa mabwawa mawili ya majitaka
  2. Ujenzi wa mabwawa mawili ya kutibu maji kibailojia
  3. Ujenzi wa Wetland kwa ajili ya kusafisha maji
  4. Ujenzi wa chambers mbili za kumwagia majitaka
  5. Ujenzi wa chambers mbili za kukausha taka ngumu na kuchoma
  6. Ujenzi wa uzio kuzunguka mabwawa ya majitaka
  7. Ununuzi wa Gari moja la majitaka

Sambamba na juhudi za Wizara kuongeza mtandao wa majitaka pia inatarajia kujenga mabwawa mengine ya majitaka maeneo ya Masimba na Igange - Malolo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bwn. Dick L. Mlimuka (Aliyesimama) kwa Niaba ya Bodi ya Wakurugenzi - TUWASA, amemshukuru sana Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya maji kwa ajili ya mradi huu wa mabwawa ya majitaka Tabora na imewasisitiza Wakandarasi kufanya kazi kwa mujibu wa Mkataba

Mgeni Rasmi Balozi Dkt. Batilda Salha Buriani alimshukuru sana Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya maji inayosimamiwa vema na Mhe. Jumaa Aweso Waziri wa Maji kwa kuboresha huduma ya majisafi Tabora na kufikia asilima 94 na sasa uboreshaji wa huduma ya majitaka unaanza. Ameeleza imani yake kubwa kwa Wizara ya maji na TUWASA kuwasimamia vizuri wakandarasi na kuhakikisha matarajio ya mradi yanafikiwa.

Aliendelea kueleza kwamba TUWASA inafanya kazi vizuri sana kwa kusimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi ya kuhudumia wananchi wa Tabora lakini wana changamoto kubwa ya madeni hasa ya Taasis za Serikali ambapo anaendelea kufuatilia. Amesisitiza wananchi kulipia huduma ya maji kwa wakati pamoja na Utunzaji  Vyanzo vya maji na miundombinu yake.